WATUMISHI WA TBC WATOA MSAADA WA MAHITAJI KWA WATOTO NJITI TUMBI.

Posted on: April 9th, 2025
Kikundi cha Misaada kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), “Mikono ya Wana” leo tarehe 9 Aprili, 2025 wametoa msaada wa mahitaji muhimu kwa mama waliojifungua watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Pwani Tumbi.
Kikundi hicho kwa niaba ya wenzao kimewashika mkono Mama waliojifungua Watoto njiti kwa kutoa Sabuni, pampasi, mafuta ya nywele na mahaitaji mengine ikiwa ni pamoja na Sukari na Pesa taslimu kwa ajili ya mahitaji ya kununulia dawa kwa watoto hao.
Akizungumza wakati wakukabidhi mahitaji hayo, Mwenyekiti wa kikundi Bwana Shamakala alisema kuwa wanajua changamoto wanazokutana nazo wamama wenye watoto njiti katika hospitali mbalimbali wanapokuwa wamelazwa na watoto hao ikiwemo uhaba wa mahitaji ya vitu kama hivyo.
Kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Pwani, Bwana Mkama Julius ambaye ni Katibu wa Afya amewashukuru wanakikundi hicho kwa kuwakumbuka wamama hao kwa kusema mahitaji hayo yatasaidia kutatua changamoto zinazowakabili wamama hao katika uhudumiaji wa watoto njiti. 
Mikono ya wana ni kikundi kinachojumuisha watumishi wa kada mbalimbali kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania chenye lengo la kutoa misaada ya mahitaji muhimu kwa jamii ya kitanzania, wakiwemo watoto yatima, wazee, wagonjwa na wengine wote wenye mahitaji maalum.