SIKU YA WAUGUZI DUNIANI

Posted on: May 28th, 2025

Leo Mei 30, 2025 Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani – Tumbi imeadhimisha siku ya Wauguzi Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 12 ya Mwezi Mei Duniani kote.

Akizungumza katika sherehe za maadhimisho hayo zilizofanyika katika Ukumbi wa B. Merlyn uliopo katika majengo ya Shirika la Elimu Tumbi, Wakati wa ukaribisho kwa wageni Mganga Mfawidhi Dkt. Amaan Malima  amesema kwamba Siku ya Wauguzi Duniani ni siku muhimu Duniani kote ambapo wanatambua, kuthamini na kusherehekea mchango mkubwa wa Wauguzi  katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.

Ameongezea kuwa kauli mbiu ya mwaka huu isemayo "Uuguzi Nguvu ya Mabadiliko" inaakisi mchango mkubwa unaotolewa na Wauguzi na kuwataka waendelee kuzingatia maadili ya taaluma yao.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho hayo ambaye ni  Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Kusirye Ukio kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchata  amesema kwamba maadhimisho ya Siku ya Wauguzi huadhimishwa tarehe 12 Mei kila mwaka Duniani kote, lakini kutokana na mwingiliano wa kazi Wauguzi wa Mkoa wa Pwani wamefanya maadhimisho haya leo Mei 30, 2025.

Aliendelea kwa kusema kwamba sekta ya Afya inayofanya shughuli za kinga na tiba asilimia kubwa ni nguvu ya Wauguzi, kwahiyo kauli mbiu ya mwaka huu tunaamini  kwamba Wauguzi wakibaki ndani ya maadili ya taaluma yao na maadili ya utumishi, kada zote za Afya wataenda kubadilika kwa kutoa huduma bora kwa mteja.


Dkt. Ukio amewakumbusha Wauguzi hao kuiga mfano wa muasisi wa huduma ya Uuguzi Florence Nightngale wa Taifa la Utaliano ambaye maadhimisho haya ya siku ya Waunguzi Duniani yanafanyika kwa ajili ya kumuenzi muasisi huyo. Amesema kwamba Wauguzi wanatakiwa kuipenda kazi yao na kuweka mazingira mazuri kwa wale wanaowategemea.

Kwa mwaka huu 2025 maadhimisho ya siku ya Wauguzi  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani  yameambatana na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchangiaji wa Damu, kutoa Elimu kuhusu Uchumi na uwekezaji kwa Watumishi  na kukabiliana na sonona mahali pa  kazi, pia maandamano  na burudani mbalimbali.